Date
Iwapo utapitishwa, mkataba wa Ushuru wa OECD/G20 utakuwa mzigo wa ziada kwa uchumi wa Afrika ambao unapata nafuu kutokana na janga la Covid-19.
Nairobi, 28 Oktoba 2021 – Nchi za Kiafrika zitafungua ukurasa mbaya wa kutoza ushuru kwa mashirika ya kimataifa isipokuwa zitakataa pendekezo la OECD/G20 la kuanzisha kiwango cha chini cha ushuru cha asilimia 15 duniani.
Bara la Afrika limekuwa likipoteza dola bilioni 89 (KES9.8 trilioni) katika kuepusha ushuru kwa utaratibu na mashirika ya kimataifa lakini kiwango cha chini cha ushuru wa kampuni cha asilimia 15, kinachotozwa kwa makampuni ambayo yanatengeneza mamilioni ya dola kwa faida kitapunguza zaidi ukusanyaji wa ushuru wa serikali za Kiafrika.
Mpango wa ushuru haujazingatia hali halisi ya mifumo ya ushuru ya nchi zinazoendelea. Takriban nchi 123, nyingi zikiwa zimeendelea, hivi majuzi ziliidhinisha pendekezo la ushuru la nguzo mbili la OECD/G20: Nguzo ya Kwanza inatenga haki za kutoza ushuru kwa “nchi za soko” ambapo mashirika ya kimataifa yanafanya kazi, na Nguzo ya Pili inaweka kiwango cha chini cha ushuru wa kampuni duniani cha asilimia 15, ambayo itatumika ambapo mashirika ya kimataifa yana makao makuu.
Zaidi ya mashirika 100 ya kiraia kutoka barani Afrika yamekosoa pendekezo la OECD/G20 na kuwataka wakuu wa nchi wa G20 kusitisha mpango huo. Kama mashirika yanayotetea haki ya kijamii, kiuchumi na kimazingira barani Afrika, yanaangazia ukosoaji ulioenea wa mpango wa ushuru wa OECD/G20.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Haki ya Ushuru Afrika, Alvin Mosioma anasema, ”Pendekezo hilo halina usawa kwa nchi zinazoendelea ambazo bado zinapata nafuu kutokana na athari za COVID-19, bila kusahau kwamba mashirika mengi ya kimataifa yanafanya matumizi mabaya ya kodi ya mashirika na sio tu kukwepa kulipa kodi, lakini pia kupuuza makubaliano ya kimazingira, mishahara na maendeleo ya jamii, hivyo kuzuia Afrika kufaidika kikamilifu na maliasili yake.”
Kwa hivyo, tunatoa mwito kwa mataifa yote yanayoendelea Kusini mwa Ulimwenguni kukataa pendekezo la OECD/G20 na badala yake kuunga mkono wito wa mchakato wa kweli unaojumuisha, wa haki, na wa kidemokrasia wa mageuzi ya kimataifa ya kodi ambapo maslahi ya mataifa yanayoendelea na bara la Afrika kuzingatiwa.
Anwani: Farah Nguegan, Meneja Mawasiliano, Barua pepe: fnguegan@taxjusticeafrica.net